Tanzania emblem

Ofisi ya Rais

Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa

Building photo

Habari

MSIANGI AWATAKA WAAJIRIWA WAPYA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA UADILIFU


MSIANGI AWATAKA WAAJIRIWA WAPYA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA UADILIFU

Na OR-IKNT

DODOMA, Septemba 3, 2026

Mkurugenzi wa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Bw. Firimin Msiangi, amewataka waajiriwa wapya kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuzingatia taratibu, maadili pamoja na miongozo ya utumishi wa umma ili kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.

Akizungumza na waajiriwa hao leo Septemba 3 wakati wa kuwapokea , Mkurugenzi Msiangi amesema ni muhimu kwa watumishi wapya kuelewa kuwa utumishi wa umma unahitaji nidhamu, uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria na kanuni zinazowaongoza katika kutekeleza majukumu yao.

Amesisitiza kuwa waajiriwa hao wanapaswa kutumia nafasi waliyopewa kwa manufaa ya taasisi na Taifa kwa ujumla, huku wakihakikisha kila jukumu wanalotekeleza linafanyika kwa uaminifu, umakini na kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma.

Aidha, amewahimiza kuendelea kujifunza na kuongeza ujuzi katika maeneo yao ya kazi, kushirikiana na watumishi wengine pamoja na kuwa tayari kupokea maelekezo na ushauri kutoka kwa viongozi na wataalamu wenye uzoefu.

“Ni wajibu wenu kufanya kazi kwa weledi, kufuata taratibu, maadili na miongozo ya utumishi wa umma na kuitumikia nchi. Nidhamu na uadilifu ni msingi wa utendaji bora na uaminifu kwa taasisi, Sitegemei kuona Mtumishi anaetokea Ofisi ya Rais ashangilie kwa kupanda juu ya meza” amesema.                                                                           

Mkurugenzi amewataka waajiriwa hao kuwa mabalozi wazuri wa Idara kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuhakikisha wanatoa huduma bora katika kila kituo walichopangiwa kufanya kazi.

Watumishi hao ni kutoka kada mbalimbali ambao wamepangiwa kazi Idarani jijini Dodoma na kanda mbalimbali za idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.