Habari
MSIANGI: USHIRIKIANO NI MSINGI WA MAFANIKIO YA IDARA
MSIANGI: USHIRIKIANO NI MSINGI WA MAFANIKIO YA IDARA
Na OR-IKNT
DODOMA, 2, Septemba, 2026
Mkurugenzi wa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin M. Msiangi, amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo kufanya kazi kwa kushirikiana, kubadilishana uzoefu na taarifa ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Idara.
Bw. Msiangi ametoa rai hiyo leo jijini Dodoma wakati akiongoza kikao cha Menejimenti cha Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
Amesema ushirikiano miongoni mwa Wakuu wa Idara na Vitengo ni muhimu katika kuhakikisha majukumu yanatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia malengo ya Idara.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya Idara yanategemea mshikamano, mawasiliano mazuri na ushirikiano wa viongozi na watumishi katika ngazi zote.
Kikao hicho cha Menejimenti kimejadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Idara, mipango ya kazi, utoaji wa huduma pamoja na hatua za kuimarisha ufanisi katika usimamizi na uhifadhi wa Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
