Habari
MAAFISA IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA, WIZARA YA AFYA WAKUTANA KUBADILISHANA UZOEFU WA MATUMIZI YA MFUMO WA E-OFFICE
MAAFISA IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA, WIZARA YA AFYA WAKUTANA KUBADILISHANA UZOEFU WA MATUMIZI YA MFUMO WA E-OFFICE
Na OR-IKNT
DODOMA, 03 SEPTEMBA, 2026
Maafisa kutoka Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa wamekutana na maafisa kutoka Wizara ya Afya kwa lengo la kubadilishana uzoefu na maarifa katika usimamizi na utunzaji wa kumbukumbu, hususan matumizi ya Mfumo wa E-Office katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Mkutano huo umejikita katika kujadili namna ya kutumia mfumo wa E-Office kwa ufanisi katika kuunda, kupokea, kusambaza, kuhifadhi na kufuatilia kumbukumbu za kiutumishi na kiutendaji, huku ukizingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka za Serikali.
Katika mkutano huo maafisa wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa walieleza umuhimu wa taasisi kuhakikisha matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaendana na taratibu za kitaalamu za usimamizi wa kumbukumbu, ili kuhakikisha kumbukumbu zinabaki kuwa salama, sahihi, kamili, zinapatikana kwa wakati na zinatunzwa kwa muda unaostahili.
Aidha, maafisa hao walisisitiza kuwa matumizi ya E-Office yanapaswa kuzingatia mzunguko mzima wa kumbukumbu, kuanzia hatua ya kuundwa au kupokelewa kwa kumbukumbu, matumizi yake, uhifadhi, ufuatiliaji hadi hatua ya mwisho ya utunzaji au uondoaji kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Kwa upande wake, Wizara ya Afya ilipata fursa ya kueleza uzoefu wake katika matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utekelezaji wa majukumu yake, pamoja na changamoto na mafanikio yanayopatikana katika usimamizi wa kumbukumbu kwa kutumia teknolojia.
Mkutano huo ni fursa muhimu kwa taasisi hizo kujifunza kutoka kwa kila upande, kuboresha matumizi ya mifumo ya kidijitali na kuimarisha usimamizi wa kumbukumbu za Serikali.
Ushirikiano huo unalenga pia kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa taarifa, kurahisisha utendaji wa kazi, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha kumbukumbu za Serikali zinalindwa na kuhifadhiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
