Tanzania emblem

Ofisi ya Rais

Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa

Building photo

Habari

TEHAMA YARAHISISHA UPATIKANAJI WA MAJARADA KUPITIA MABADILIKO YA NAKALA NGUMU KWENDA NAKALA LAINI


TEHAMA YARAHISISHA UPATIKANAJI WA MAJARADA KUPITIA MABADILIKO YA NAKALA NGUMU KWENDA NAKALA LAINI

Na OR-IKNT

MWANZA, 16 NOVEMBA, 2026

Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanaendelea kuboresha usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka kwa kurahisisha upatikanaji wa majarada kupitia mabadiliko ya mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu kutoka nakala ngumu kwenda nakala laini (kidijitali), hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kuharakisha utoaji wa huduma kwa watumishi, taasisi na wananchi kwa ujumla.

Mbali na jukumu la kutunza na kuhifadhi Nyaraka mbalimbali, wataalamu wa kumbukumbu wana wajibu wa kuhakikisha nyaraka hizo zinapatikana kwa urahisi na kwa wakati zinapohitajika kwa matumizi mbalimbali. Hivyo, matumizi ya TEHAMA yamekuwa nyenzo muhimu katika kufanikisha jukumu hilo.

Akielezea namna teknolojia hiyo inavyorahisisha utekelezaji wa majukumu katika Kituo cha Kanda ya Ziwa, Afisa Kumbukumbu, Bi. Joyce Katabarwa, amesema kuwa uwekaji wa majarada katika mfumo wa nakala laini unarahisisha upatikanaji wake wakati wa kutoa huduma kwa watumishi, taasisi na wananchi.

“Tunaweka majarada katika mfumo wa nakala laini ili kurahisisha upatikanaji wake wakati wa kuwahudumia watumishi, taasisi na wananchi kwa ujumla,” amesema Katabarwa.

Kwa upande wake, Afisa Kumbukumbu katika kituo hicho, Bw. Augustine Luando, amesema kuwa matumizi ya mfumo huo yamerahisisha pia upatikanaji wa nyaraka zinazohitajika na taasisi mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya rejea.

Amesema awali kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa nyaraka hizo kutokana na kutokuwepo kwa orodha iliyokamilika ya majarada, hali iliyosababisha taasisi zinazohitaji nyaraka husika kutumia muda mrefu kuzitafuta.

“Mwanzo tulikuwa tunapata changamoto kwa sababu hatukuwa tumeandaa orodha ya majarada, na taasisi zilizokuwa zikihitaji nyaraka hizo pia hazikuwa na orodha. Hali hiyo ilifanya upatikanaji wa nyaraka walizohitaji kuwa mgumu na kuchukua muda mrefu,” amesema Luando.

Mabadiliko hayo yanaonesha umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuboresha mifumo ya usimamizi wa kumbukumbu, kwani yanasaidia kupunguza muda wa kutafuta majarada, kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Aidha, matumizi ya mfumo wa kidijitali yanachangia kuboresha usimamizi wa nyaraka, kurahisisha ufuatiliaji wake na kupunguza utegemezi wa nakala za karatasi, huku yakihakikisha taarifa zinapatikana kwa wakati zinapohitajika.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa za kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka, ili kuboresha upatikanaji wa taarifa na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa umma.