Habari
UPATIKANAJI WA TAARIFA MUHIMU KWA WAKATI WARAHISISHA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU KWA WATENDAJI
UPATIKANAJI WA TAARIFA MUHIMU KWA WAKATI WARAHISISHA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU KWA WATENDAJI
Na OR-IKNT
MWANZA, 13 NOVEMBA,2026
Upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wakati ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuongeza ufanisi, kurahisisha maamuzi na kuboresha utekelezaji wa majukumu kwa watendaji katika taasisi za umma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kanda ya Ziwa, Bi. Saida Mohamed, wakati wa Kikao cha Kawaida cha Watendaji wa Idara ya Kumbukumbu, Kanda ya Ziwa, ambapo amesisitiza umuhimu wa watendaji kupata taarifa sahihi na kwa wakati ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa.
Amesema kuwa ukosefu wa taarifa muhimu kwa wakati unaweza kusababisha ucheleweshaji wa shughuli za kikazi, kufanya maamuzi kuwa magumu na kuathiri utekelezaji wa mipango na majukumu yaliyopangwa.
Aidha, Bi. Saida ameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kusogeza huduma za Kumbukumbu karibu na wananchi kwa kuanzisha vituo vya huduma katika mikoa, akieleza kuwa hatua hiyo imekuwa na manufaa kwa watumishi wa Serikali, wananchi na watafiti ambao sasa wanapata huduma kwa urahisi zaidi.
Ameongeza kuwa uwepo wa huduma hizo katika Kanda ya Ziwa umesaidia kurahisisha upatikanaji wa taarifa na nyaraka muhimu zinazohitajika kwa matumizi mbalimbali ya kiutendaji na kiutafiti.
Amesisitiza kuwa watendaji wanapaswa kuendelea kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha taarifa na nyaraka muhimu zinapatikana na kutolewa kwa wakati ili kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu ya Idara.
