Tanzania emblem

Ofisi ya Rais

Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa

Building photo

Habari

WATANZANIA WENGI WANAPATA HUDUMA KATIKA IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA


WATANZANIA WENGI WANAPATA HUDUMA KATIKA IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA

Na OR-IKNT

DODOMA, Agosti 19, 2026

Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imeendelea kutoa huduma kwa Watanzania na watafiti kutoka ndani na nje ya nchi, huku idadi ya watafiti wa ndani ikiongezeka kutokana na kuimarika kwa uelewa kuhusu umuhimu wa nyaraka za kitaifa.

Akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Idara hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Nyaraka, Bw. Athanas Bernad Kolokota, amesema moja ya majukumu makuu ya Idara ni kukusanya na kuhifadhi nyaraka kutoka taasisi za umma na binafsi, pamoja na nyaraka zinazomilikiwa na watu binafsi ambazo zina umuhimu mkubwa kwa taifa.

Kazi ya Idara hii ninayoiongoza ni kukusanya nyaraka mbalimbali kutoka taasisi za umma na binafsi, kigezo kikubwa kikiwa ni kwamba nyaraka hizo ziwe na umuhimu mkubwa kitaifa. Hivi karibuni tumewafikia watu binafsi na kuhifadhi nyaraka kutoka kwa Kanyama Chiume, Shaaban Robert na wengineo,” alisema.

Aliongeza kuwa Idara hiyo pia ina jukumu la kuwahudumia watafiti wa ndani na nje ya nchi, kufanya ukarabati wa nyaraka zilizohifadhiwa pamoja na kuuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kutunza na kuhifadhi nyaraka zenye thamani ya kitaifa.

Kwa mujibu wa Kolokota, nyaraka zinazohifadhiwa na Idara hiyo zina historia ya muda mrefu, zikiwemo nyaraka za kipindi cha utawala wa Kijerumani, Waingereza na nyaraka za kipindi cha sasa.

Hapa tuna nyaraka za tangu enzi za Mjerumani, Mwingereza na hata za sasa,” alisema.

Aidha, Kolokota alisema kuwa kwa miaka ya nyuma Idara ilikuwa ikipokea watafiti wengi kutoka nje ya nchi, lakini hali imeanza kubadilika ambapo watafiti wa ndani wameongezeka kutokana na kuimarika kwa uelewa wa Watanzania kuhusu thamani ya nyaraka katika tafiti na maendeleo ya taifa.

Kwa zamani, Idara yetu ilikuwa inapokea watafiti wengi kutoka nje ya nchi, lakini sasa watafiti wa ndani wamekuwa wengi zaidi kutokana na uelewa kuwa mkubwa kwa Watanzania. Hivyo, nahimiza kila mmoja wetu atunze nyaraka hizo, na Idara yetu ni yetu sote,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma za Kumbukumbu, Ndugu Emilios Muungano, alieleza utaratibu unaotumika kwa watafiti wanaofika katika Idara hiyo kwa ajili ya kupata huduma.

Alisema watafiti kutoka nje ya nchi hupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kabla ya kufika katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, huku Watanzania wakipata huduma hizo bila malipo kwa kuwasilisha barua za utambulisho au vitambulisho vinavyotambulika, ikiwemo NIDA.

Huduma zetu hutolewa baada ya kila mtafiti kutoka nje ya nchi kupitia COSTECH, kisha kufika hapa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa. Hii ni kwa wageni, lakini kwa sisi Watanzania huduma hii hutolewa bure wanapokuwa na barua za utambulisho au vitambulisho kama vile NIDA, na huwa hawalipi gharama yoyote ile,” alisema Muungano.

Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa inahimiza wananchi kutambua umuhimu wa kuhifadhi nyaraka zinazobeba historia ya familia, taasisi na taifa kwa ujumla, na kuzifikisha katika Idara pale zinapokuwa na thamani ya kihistoria na kitaifa.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha urithi wa nyaraka za Tanzania unalindwa na kuendelea kuwa chanzo muhimu cha taarifa kwa watafiti, taasisi na wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.