Habari
MHADHIRI WA UDSM, MDAU WETU KATIKA JUMA LA HUDUMA KWA WATEJA
MHADHIRI WA UDSM, MDAU WETU KATIKA JUMA LA HUDUMA KWA WATEJA
OR-IKNT
Dodoma, Oktoba 7, 2026
Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, ilimpokea mtafiti na Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mtechura Brighton, anayefanya utafiti kuhusu masuala ya utamaduni na filamu nchini Tanzania.
Akiwa katika Ofisi za Idra hii jijini Dodoma, Mtechura alihudumiwa na Bi. Leaclara Ngair, Afisa Kumbukumbu katika taasisi hii.
Tukio hili limefanyika wakati wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, inayoadhimishwa mwaka huu kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026, ikiwa na lengo la kutambua umuhimu wa kutoa huduma bora, zenye ufanisi na zinayozingatia mahitaji ya wateja.
Akiwa hapa, yalifanyika mazungumzo mbalimbali yaliyolenga zaidi sekta ya filamu nchini Tanzania, historia yake, maendeleo ya kiteknolojia pamoja na changamoto zinazokabili sekta hiyo katika kipindi cha sasa.
Akizungumzia hali ya sekta ya filamu nchini, Mtechura alisema kuwa sekta hiyo imepiga hatua katika maeneo mbalimbali, hususan kutokana na maendeleo ya teknolojia. Hata hivyo, alieleza kuwa mabadiliko hayo yameambatana na changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele.
“Sekta ya filamu nchini Tanzania imepiga hatua kadhaa. Japokuwa sasa kuna maendeleo makubwa ya teknolojia, hali ya filamu hapo awali ilikuwa nzuri na ilikuwa katika mikono salama, hasa kwa kuzingatia maadili, mila na tamaduni za taifa. Lakini kwa sasa, milango ya soko huria la filamu imeruhusu mambo mazuri na mabaya kuingia. Kwa sasa, sekta ya filamu ipo katika hali inayohitaji umakini zaidi.”Alisema ndugu Mtechura.
Akizungumzia utafiti anaoufanya, Mtechura alisema kuwa tayari amefanikiwa kupata maarifa na taarifa mbalimbali ambazo zitasaidia katika kukamilisha kazi yake.
“Nimefanikiwa kuyafahamu mengi katika tafiti zangu, na naamini mara baada ya kumaliza utafiti huu, mengi nitayaweka bayana. Nashukuru sana Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, kwa kutunza kumbukumbu vizuri. Kumbukumbu hizi ni utajiri wa miaka mingi ambao una umuhimu mkubwa kwa watafiti na taifa kwa ujumla.”
Wiki ya Huduma kwa Wateja, kwa Kiingereza Customer Service Week, ilianzishwa mwaka 1984 nchini Marekani na International Customer Service Association (ICSA). Baadaye, mwaka 1992, ilitambuliwa rasmi na Bunge la Marekani kama tukio la kitaifa na kupewa nafasi ya kuadhimishwa katika wiki ya kwanza kamili ya Oktoba kila mwaka.
Kwa miaka ya hivi karibuni, Wiki ya Huduma kwa Wateja imeendelea kuadhimishwa katika nchi mbalimbali duniani, ikiwemo nchi za Afrika, kwa lengo la kuhamasisha taasisi na mashirika kuweka mkazo katika ubora wa huduma wanazowapatia wateja.
Kwa mwaka 2026, Wiki ya Huduma kwa Wateja inaadhimishwa kuanzia Oktoba 5 hadi 9.
Wiki ya Huduma kwa Wateja barani Afrika
Katika bara la Afrika, maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yameendelea kuenea katika nchi mbalimbali kadiri dhana ya huduma bora kwa wateja ilivyozidi kupewa umuhimu, hususan katika sekta binafsi na taasisi zinazotoa huduma moja kwa moja kwa wananchi.
Nchini Nigeria, kuna kumbukumbu za shughuli za Wiki ya Huduma kwa Wateja zilizohusishwa na mwaka 2005, huku Ghana ikiwa miongoni mwa nchi zilizokuja kuwa na mpango rasmi wa kitaifa wa kuhamasisha maadhimisho hayo mwaka 2011.
Kwa upande wa Tanzania, maadhimisho hayo yamekuwa yakionekana zaidi katika taasisi na mashirika mbalimbali, hususan katika sekta binafsi kama vile benki na taasisi nyingine za huduma, kuanzia miaka ya 2000. Hata hivyo, historia rasmi ya mwaka ambao Tanzania ilianza kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kiwango cha kitaifa bado inahitaji kumbukumbu na chanzo rasmi cha kitaifa.
Uwepo wa mtafiti Mtechura katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa juma hili unaonesha umuhimu wa taasisi hii katika kuhifadhi historia na taarifa ambazo zinaweza kutumika na watafiti, wanataaluma, watunga sera na wananchi kwa ujumla.
Katika kipindi ambacho teknolojia inabadilisha kwa kasi namna taarifa zinavyotengenezwa, kuhifadhiwa na kusambazwa, uwepo wa kumbukumbu salama na zinazopatikana kwa urahisi ni muhimu katika kuhakikisha historia ya taifa, utamaduni na maendeleo yake inalindwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Huduma bora kwa mteja si kumhudumia tu anayefika katika ofisi, bali pia kuhakikisha anapata taarifa sahihi, mazingira rafiki na huduma inayokidhi mahitaji yake.
