Habari
MAWASILIANO BORA, WELEDI NA UWAJIBIKAJI NGUZO ZA UTENDAJI IMARA
MAWASILIANO BORA, WELEDI NA UWAJIBIKAJI NGUZO ZA UTENDAJI IMARA
OR-IKNT
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi, amewahimiza watumishi wa Idara hii kuzingatia weledi, uwajibikaji na mawasiliano yenye ufanisi katika kutekeleza majukumu yao, ili kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wakati wa kutoa huduma.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma tarehe 9 Oktoba 2026, wakati wa kikao kazi cha utendaji kilicholenga kuboresha utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa Idara.
Akizungumza katika kikao hiki, Msiangi ameeleza kuwa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ina nafasi muhimu katika utendaji wa taasisi za umma, kutokana na mchango wa watumishi wake katika usimamizi wa shughuli za kiutawala, uendeshaji wa ofisi na kutunza kumbukumbu.
“Idara yetu ni moyo wa taifa, maana katika kila taasisi ya umma tunawakilishwa vizuri na Waandishi Waendeshaji Ofisi na Watunzaji Kumbukumbu,” amesema Msiangi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya mara kwa mara na kwa wakati ,kati ya wakuu wa idara na vitengo pamoja na watumishi walio chini yao, na kusema kuwa mawasiliano bora ni nyenzo muhimu katika kuratibu shughuli, kutatua changamoto na kuhakikisha majukumu yanatekelezwa kwa wakati.
Msiangi amewataka watumishi kuzingatia matokeo ya kazi wanazotekeleza, badala ya kujikita katika kueleza hatua na michakato ya utekelezaji bila kuonesha mafanikio yaliyopatikana.
“Katika utendaji kazi bora, tunatakiwa kuripoti matokeo baada ya kukamilisha kazi na siyo kuripoti michakato. Kazi zote zifanyike kwa kuzingatia mifumo na maelekezo yote ya Serikali,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa uzingatiaji wa mifumo, taratibu na maelekezo ya Serikali, sambamba na kuimarisha uwajibikaji na mawasiliano mahali pa kazi, ni muhimu katika kufanikisha malengo ya Idara na kuboresha utendaji wa taasisi za umma.
Kikao hiki ni sehemu ya jitihada za kuimarisha usimamizi wa majukumu na kuhamasisha watumishi kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa katika utumishi wa umma.
